Na Lucas Mboje, Ludewa

KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike ameahidi kulipatia trekta moja Gereza la Kilimo Ludewa ili kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa.

Kamishna Jenerali Kasike ametoa ahadi hiyo leo wakati akizungumza na uongozi wa Gereza hilo baada ya kuwasili Wilayani Ludewa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Amesema kuwa Gereza Ludewa ni miongoni mwa magereza 13 ambayo tayari yameainishwa katika mpango mkakati wa Jeshi la Magereza katika kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa waliopo magerezani hivyo lazima liwezeshwe zana za kilimo.

“Nafahamu kuwa trekta lililopo hapa Gereza Ludewa ni la muda mrefu na ni chakavu, hivyo nitawapatieni trekta jipya ili muweze kuongeza uzalishaji wa chakula cha wafungwa”. Alisema Jenerali Kasike.

Pia, Kamishna Jenerali Kasike amehimiza uongozi wa Gereza hilo kuzingatia suala zima la uadilifu na amewataka kujiepushe na vitendo vyote vya ubadhilifu wa mali za umma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza hilo, SSP. Akley Mkude amesema kuwa  katika msimu wa Kilimo wa mwaka 2017/2018 gereza hilo lililima ekari 200 za mahindi na kufanikiwa kuvuna gunia zaidi ya 1700 ambazo zitatumika kulisha magereza yote ya Mkoa wa Njombe na Iringa.

Aidha, ameongeza kuwa  malengo ya msimu huu wa mwaka 2018/2019 ni kulima ekari 700 za mahindi, ekari 40 za maharage, ekari 30 za alizaeti pamoja na bustani ekari 5 za mbogamboga.

Gereza Ludewa lina eneo lenye ukubwa wa ekari 3500, Gereza hilo linajishughulisha na kilimo cha mahindi, maharage, alizeti pamoja na bustani za mbogamboga. Pia, linajishughulisha na miradi ya ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kuku wa kienyeji pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com