Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP)  Phaustine Kasike akisalimiana na Meneja Miradi wa Asasi ya Kidini ya New Life In Christ Ndg. Charles Shang’a mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga Moshi kwa ajili ya hafla fupi ya kupokea Misaada ya Kibinadamu iliyotolewa na Asasi hiyo kwa ajili ya  wafungwa  leo Septemba 8, 2018

 

Na Deodatus Kazinja

Wito umetolewa kwa Asasi mbalimbali za kiraia kujitokeza kushirikiana na Jeshi la Magereza  nchini katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazoweza kulikwamisha katika kutoa huduma muhimu za wafungwa kutokana na ufinyu wa bajeti.

Hayo yamesemwa leo na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Phaustine Kasike katika hafla ya kupokea msaada wa Kibinadamu uliotolewa na Asasi ya Kidini ya New Life In Christ  iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu Karanga mjini Moshi leo Septemba 8, 2018.

“Ni ukweli usiopingika kuwa Jeshi la Magereza limekuwa likishindwa kutekeleza kwa ukamilifu utoaji wa baadhi ya huduma muhimu kwa wafungwa kutokana na ufinyu wa bajeti” Amesema Kamishna Jenerali Kasike

Na kuongeza “ natoa wito kwa Asasi nyingine kuiga mfano uliooneshwa na New Life in Christ na Dorcas Aid International Tanzania zinavyoshirikiana na Jeshi la Magereza”
Asasi ya Kidini ya New Life In Christ  pamoja na Dorcas Aid International Tanzania kwa miaka 14 sasa tangu 2005 zimekuwa zikishirikiana na Jeshi la Magereza kwa kutoa misaada ya Kibinadamu na Kiroho yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.7.

Kwa kipindi chote hicho Asasi hizi zimekuwa zimekuwa zikitoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezeshaji wa semina za ushauri pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa wafungwa na maafisa wa magereza.

Huduma nyingine ni kuwa na vituo vidogo vidogo vya kujifunza kufanya jambo ambavyo tayari linafanyika ndani ya magereza kama vile uokaji mikate, ushonaji na kudarizi, ushonaji wa viatu, ukinyozi,useremala na uchomeleaji mchanganyiko.

Katika hafla hiyo Asasi ya Kidini ya New Life In Christ imekabidhi msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.2. Na kuahidi kuendelea kutoa misaada ya namna hiyo kwa kadiri Mungu atakavyowajali.

Misaada ya Kibinadamu iliyotolewa leo imewalenga zaidi wafungwa walioko mkoani Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Mwanza. Ambapo Kamishna Kasike amewaagiza wakuu  wa magereza yote ambayo vifaa hivyo vitapelekwa kuhakikisha wanavitunza na kuvitumia kwa uadilifu kama ilivyokusudiwa.

 

Kwa habari picha zaidi tembelea www.magereza.blogspot.com