Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike akitoa hotuba wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa zahanati ya gereza la Mahabusu Morogoro  Julai 27, 2018.

 

Na Mwandishi wetu
Watendaji wote ndani ya Jeshi la Magereza wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kupokea mkakati maalum wa uzalishaji chakula unaolenga kujitosheleza kwa chakula cha wafungwa na ziada kuuzwa katika sehemu nyingine.

Hayo yalisemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini Phaustine Kasike alipokuwa akizungumza na maafisa, askari na watumishi raia wa jeshi hilo alipofanya ziara yake ya kwanza mkoani Morogoro tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Julai 13 mwaka huu.
Kamishna Jenerali Kasike alisema maandalizi ya mkakati huo yanaendelea vizuri makao makuu ya jeshi hilo na katika kipindi kifupi kijacho maelekezo ya utekelezaji wake yatatolewa na kushushwa katika vituo vyote vya magereza kwa ngazi ya mikoa na wilaya.

Alisema mkakati huu utakapokuwa umekamilika itakuwa ndiyo dira ya utekelezaji ndani ya na utamtaka kila kiongozi kuwa na mpango kazi katika eneo lake unaokwenda sambamba na malengo mapana ya jeshi hilo.

“Ninaamini jambo hili linawezekana na kwa kuanza na raslimali chache zilizopo kwakuwa wataalam wapo, ardhi ipo na nyenzo za kuanzia zipo tukijipanga vizuri tunaweza kupata mahala pazuri pa kuanzia” Alisema Jenerali Kasike

Na kuongeza “ miongoni mwa taasisi zenye wasomi wazuri katika maeneo mengi ni pamoja na jeshi letu la Magereza, sasa umefika wakati wa kuona wataalam hawa wanatumika ipasavyo na wanaleta tija jeshini na taifa kwa ujumla”

Pamoja na mambo mengine Kamishna Kasike aliwataka watumishi wa jeshi hilo kote nchini kubadili mtazamo wa namna wanavyofanya kazi kwa kusoma alama za nyakati na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kamishna Kasike alisema ifike mahala kila mmoja asijikie aibu na fedheha kuona jeshi letu linasemwa vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hata katika mambo ambayo yako ndani ya uwezo wa watendaji wenyewe.

Akitolea mfano wa uingizwaji wa vitu visivyoruhusiwa magereza kama vile simu, bangi, pesa nakadhalika Kamishna Kasike alisema hivi havihitaji bajeti kuviondoa ni kiasi cha watendaji kubadilika tu.

“ Hapa kuna tatizo kubwa la kimaadili, badilikeni. Nitakuwa mkali sana. Askari asiyekuwa na maadili na nidhamu hawezi kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Nimeanza kwa kuwaeleza ili nieleweke vizuri hatua nitakazozichukua kwa yeyote asiyetaka kubadilika” Alisisitiza Kamishna Kasike.
Kamishna Kasike aliwaambia kuwa anatambua uwepo wa changamoto kadhaa kama vile ukosefu wa nyumba na zilizopo kuchakata, ukosefu mkubwa wa vyombo vya usafiri, malimbikizo ya madeni, kutopandishwa vyeo kwa wakati, uhaba wa sare na mengine.

Amewahakikishia kuwa serikali inayatambua yote na tayari imeanza kuchukua hatua katika baadhi ya mambo na kuwaomba ushirikiano wakati yeye akiwa mtendaji mkuu anafanya ufuatiliaji.

Ziara ya Kamishna Jenerali Kasike ilimfikisha katika gereza la Mahabusu Morogoro ambapo alizindua zahanati ya gereza hilo, kuongea na maafisa na askari wa gereza Kihonda, Kingolwira Complex inayoundwa na vituo vya Chuo cha Ufundi KPF,Gereza Mtego wa Simba, Mkono wa Mara na Gereza Kuu la Wanawake.

Pia Jenerali Kasike alitembelea mashamba ya miwa inayolimwa katika eneo la gereza Mbigiri wilaya ya Mvomero chini ya mradi wa ubia wa kuzalisha sukari kati ya Magereza na mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PPF na NSSF. 

 Kwa habari picha zaidi, tembelea www.magereza.blogspot.com